Serikali ya Sudan Kusini imetangaza kuwa, mazungumzo yake na waasi
wanaoongozwa na aliyekuwa Makamu wa Rais Riek Machar yanakabiliwa na
vizingiti vigumu. Msemaji wa timu ya serikali katika mazungumzo na waasi
Michael Makuei amebainisha kuwa, waasi wa nchi hiyo wamekuja na mambo
mapya jambo ambalo limeufanya mwenendo wa mazungumzo hayo kukabiliwa na
kikwazo. Afisa huyo mwandamizi katika mazungumzo na waasi amesisitiza
kuwa, waasi hao hawako makini katika mazungumzo na wanataka kuvunjwa
Bunge na asasi nyingine hususan Kamisheni ya Taifa ya Uchaguzi,
Kamisheni ya Taifa ya Kutazama Upya Katiba, vyombo vya mahakama na
kubadilishwa wajumbe na viongozi wote wa taasisi hizo.Wakati huo huo Pout Kang, msemaji wa waasi wa Sudan Kusini ametangaza kuwa, hawajafikia makubaliano yoyote yale na serikali ya Juba. Hayo yanajiri katika hali ambayo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hivi karibuni liliunga mkono azimio la kuziwekea vikwazo pande mbili hasimu za Sudan Kusini, endapo hazitafikia makubaliano katika muda ulioainishwa ambao ulimalizika jana.



0 comments:
Post a Comment