Siku kama ya leo miaka 9
iliyopita, Slobodan Milosevic dikteta wa Yugoslavia ya zamani aliaga
dunia akiwa korokoroni mjini Hague huko Uholanzi. Milosevic alitiwa
mbaroni mwaka 2001 miezi tisa baada ya kuanguka utawala wake na
kukabidhiwa kwa mahakama ya watenda jinai wa Yugoslavia ya zamani huko
Hague. Slobodan Milosevic alijiunga na chama cha Kikomonisti cha
Yugoslavia ya zamani akiwa kijana na kuwa Rais wa Jamhuri ya Serbia
mwaka 1989. Dikteta huyo wa Yugoslavia ya zamani alikuwa akikabiliwa na
tuhuma za kushiriki katika mauaji ya umati dhidi ya maelfu ya Waislamu
wa Bosnia.
Miaka 11 iliyopita katika siku
inayosadifiana na ya leo, miripuko ya mabomu matano ilitokea kwa wakati
mmoja katika vituo kadhaa vya treni za chini ya ardhi au metro huko
Madrid mji mkuu wa Uhispania na kuua karibu watu 200 na kujeruhi wengine
1000. Miripuko hiyo ilitambuliwa kuwa operesheni kubwa zaidi ya kigaidi
kuwahi kutokea nchini Uhispania na Ulaya baada ya Vita vya Pili vya
Dunia. Japokuwa serikali ya mrengo wa kulia ya Uhispania ililituhumu
kundi linalotaka kujitenga eneo la Basque la ETA kuwa ndilo lililohusika
na mashambulizi hayo ya kigaidi lakini kundi la al Qaida lilitoa
taarifa likisema kuwa ndilo lililotekeleza hujuma hiyo.
Na miaka 30 iliyopita katika
siku inayosadifiana na hii ya leo, mgogoro mkubwa katika ngazi za
uongozi wa Urusi ya zamani ulifikia kikomo kufuatia kutangazwa kifo cha
Konstantin Chernenko na badala yake Mikhail Gorbachev ambaye wakati huo
alikuwa mwanachama kijana zaidi katika ofisi ya kisiasa ya chama cha
Kikomunisti akatangazwa kuchukua nafasi ya Chernenko. Hatua ya
kuchaguliwa Gorbachev kuongoza chama hicho cha Kikomunisti ilikwenda
sambamba na kujiri mabadiliko makubwa, ambayo hatimaye yalipelekea
kusambaratika Umoja wa Kisovieti.
0 comments:
Post a Comment