Dar es Salaam. Shirika la Umeme (Tanesco) limesema limbikizo la
deni la Sh275 bilioni kwa taasisi mbalimbali za Serikali na wateja
binafsi, linachangia kukwamisha utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Hata hivyo, Tanesco imeelezwa kuwa deni hilo
limeanza kupunguzwa na mpaka kufikia Juni, mwaka huu, takriban Sh30
bilioni zilikwishalipwa na wadaiwa.
Kutokana na ukosefu wa fedha, Tanesco inafanya
juhudi za ziada ili kufanyia matengenezo transfoma inayosambaza umeme
katika eneo kubwa la Kipawa jijini.
Akizungumza jana na gazeti hili, msemaji wa
shirika hilo, Adrian Severin alisema hutamani kufanya kazi bila kuwakera
wateja wao, lakini tatizo la fedha linawafanya washindwe kufikia
malengo.
Hata hivyo, Severin alisema baada ya kufikia
kikomo cha muda wa tangazo la ukusanyaji wa madeni hayo, Tanesco itaanza
kuchukua hatua kali dhidi ya wadaiwa wote sugu.
“Kuna ripoti ambayo tutaipokea leo (jana)
itakayokuwa na mwelekeo wa jinsi gani tutakusanya madeni hayo.
Inasikitisha kuona taasisi za Serikali na wateja wengine hawalipi madeni
yao wakati wanaendelea kupata huduma,” alisema.
“Shirika linaathirika sana na deni hilo,
tunashindwa kutoa huduma kwa ufanisi katika maeneo mengi kwa sababu ya
kukosa fedha. Kiasi hicho kama kingekuwapo kingeweza kusaidia kutatua
changamoto hizi ambazo kwa kweli ni kero kubwa kwa wateja wengine.”
Akizungumzia transfoma ya Kipawa, Severin alisema
mainjinia wa Tanesco wamebaini tatizo kubwa ambalo litatatuliwa baada ya
siku tatu mpaka nne.
“Kuna mtaalamu atafika leo (tangu jana) kutoka
India kwa ajili ya kuitengeneza. Inaweza kukamilika Jumatano au
Alhamisi,” alisema alisema Severin.
Alisema kuharibika kwa transfoma hiyo, kumeyafanya
maeneo ya Kisarawe, Gongo la Mboto, Kivule, Kipunguni, Ukonga, Tabata,
Uwanja wa Ndege, Chang’ombe, Tandika, Nyerere Road na maeneo jirani
kukosa umeme.
Alisema ili kupunguza usumbufu, umeme unaotumiwa
katika makazi ya watu kwa sasa utatoka katika transfoma ya Ubungo,
“lakini kwa viwanda itabidi wasubiri mpaka matengenezo yatapokamilika.”
0 comments:
Post a Comment