Rais Jakaya Kikwete(katikati), akiwa na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), alipotembelea banda la mamlaka hiyo kwenye Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) juzi. Wa nne kulia ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Rished Bade. Picha na Ikulu.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), imesema matumizi ya mfumo mpya wa kuratibu mizigo inayotoka nje
kuingia nchini utakuwa njia bora katika kuharakisha utoaji wa mizigo
hiyo mara inapoingia.
Hayo yalisemwa juzi na Kamishna Mkuu wa TRA,
Rished Bade wakati akimtembeza Rais Jakaya Kikwete katika idara
mbalimbali za mamlaka hiyo katika maonyesho ya Sabasaba.
“Tunatarajia mfumo huu utaongeza ufanisi wa
ukusanyaji wa kodi na kuharakisha clearance (utoaji wa mizigo kutoka
nje), wataalamu wangu watakueleza jinsi unavyofanya kazi na faida zake
kwa wadau mbalimbali,” alisema Bade.
Ofisa Msaidizi wa Huduma na Elimu kwa MlipaKodi,
Chama Siriwa akitoa maelezo ya utendaji kazi wa mfumo huo ujulikanao
kama TanCIS (Tanzania Customs Integrated System) alisema mpaka sasa
tayari shughuli mbili zinaratibiwa chini ya mfumo huo.
“Tayari tunafanya cargo management (usimamizi wa
mizigo) tangu Oktoba mwaka jana pamoja na clearance (kuondoa mizigo
bandarini) tuliyoanza kuifanya Aprili Mosi, mwaka huu.
Ni mfumo uliounganishwa na mifumo mingine hivyo kurahisisha usalama na kazi nzima ya utoaji wa mizigo bandarini, alisema Siriwa.
“Huu mfumo mpya utasaidia upataji wa taarifa kwa
wakati miongoni mwa wadau. Hata mawakala wanautumia katika utoaji wa
mizigo…waagizaji wa mizigo vilevile wataweza kuangalia mizigo yao
imefikia hatua ipi na pia kujua imehifadhiwa sehemu gani,” alisema
Siriwa na kubainisha kuwa ni mteja mwenye mzigo pekee atakayeruhusiwa
kujua hilo kwa kutumia namba yake ya BL ili kuepusha wizi unaoweza
kujitokeza.
Kwa hatua ya mwanzo, kuanzia Julai Mosi, mwaka
huu, mawakala wote wa Dar es Salaam wamesajiliwa kabla ya kuwahusisha na
wale wa mikoani katika mfumo huo unaoruhusu wakala kukadiria kodi na
mteja kuilipa kabla mzigo huo haujafika nchini.
“Kama taarifa za wakala zitalingana na manifest
(nyaraka za usafirishaji) basi ataruhusiwa kutoa mzigo wake baada ya
kulipa gharama zinazostahili tofauti na zamani ambapo tulikuwa
tunasubiri mpaka shiper (msafirishaji) alete hiyo manifest,” alisema
Siriwa.
0 comments:
Post a Comment