Rais Idriss Derby wa Chad hivi karibuni
alisisitiza suala la kuangamizwa kikamilifu kundi la kigaidi la Boko
Haram. Baadhi ya wapembuzi wa mambo wameitathmini hatua ya Rais Derby
kutuma mapema vikosi vya jeshi katika mpaka wa nchi za Nigeria na
Cameroon kuwa ni katika jitihada za kiongozi huyo za kutaka kuwa na
nafasi muhimu katika eneo hilo. Serikali ya Nigeria nayo imetoa
radiamali kali kuhusu suala la kutumwa wanajeshi wa Chad katika maeneo
ya mipaka ya pamoja ya nchi hizo. Radiamali hiyo imetokana na wasiwasi
wa serikali ya Nigeria kuhusu uwezekano wa Chad kuwa na ushawaishi na
kuingia katika ardhi yake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
Umoja wa Afrika, vikosi hivyo vya muungano wa jeshi la kieneo
havitaingia katika ardhi ya Nigeria, bali vitapelekwa katika maeneo
yanayolizunguka ziwa Chad.
Wasiwasi wa serikali ya Nigeria kuhusu
suala la kutumwa nchini humo vikosi vya kigeni katika kipindi hiki cha
kukaribia uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika katika miezi ya Machi na
Aprili mwaka huu ni jambo linaloweza kueleweka.
Wataalamu ya masuala ya kiusalama
walitahadharisha kuwa, mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram
yataongezeka sambamba na kukaribia wakati wa kufanyika uchaguzi nchini
Nigeria. Inaonekana kuwa, makubaliano yaliyofikiwa kati ya vyama kumi
vya kisiasa kwa ajili ya kuzuia ghasia za uchaguzi, yatapunguza wasiwasi
uliojitokeza ndani ya nchi hiyo. Pamoja na hayo yote, wasiwasi kuhusu
harakati za kundi la kigaidi la Boko Haram utaendelea kuwapo, iwapo
vyanzo vya fedha na silaha zinazohitajika kwa ajili ya kuanza operesheni
ya jeshi dhidi ya Boko Haram havitaweza kudhaminiwa.
Ostia Chidoka ambaye ni mshauri wa Rais
Goodluck Jonathan wa Nigeria ametahadharisha kuwa, nchi za Magharibi pia
zitakabiliwa na hatari ya kundi la kigaidi la Boko Haram. Kwa mtazamo
huo, iwapo jamii ya kimataifa haitaiunga mkono kifedha na kisilaha
serikali na jeshi la Nigeria katika operesheni ya kuliangamiza kundi la
Boko Haram, mashambulizi ya kundi hilo la kigaidi yatavuka mipaka ya
Nigeria na Afrika na kuzitishia nchi za bara Ulaya kama Uingereza. Hatua
ya wanamgambo wa Boko Haram ya kuiga vitendo vya ukatili vya kundi la
kigaidi la Daesh kama kuwauwa watu kwa kuwakata vichwa, inatia nguvu
dhana hiyo.
Weledi wa mambo wanaamini kuwa matamshi
ya mshauri wa Rais wa Nigeria yumkini yakawa na ukweli. Pamoja na hayo
yumkini tahadhari hiyo ikawa na lengo la kuvutia fikra za waliowengi
duniani, ambao macho na masikio yao wameelekezwa kwenye matukio
yanayojiri ndani ya Syria na Iraq kuhusiana na jinai na ukatili
unaofanywa na kundi la kigaidi la Daesh. Uwezekano mwingine ni kuwa,
tahadhari ya Ostia Chidoka ni aina fulani ya kuziomba msaada nchi za
Magharibi kama Marekani na Uingereza kwa ajili ya kupambana na Boko
Haram.
Goodluck Jonathan, mgombea wa chama
tawala katika uchaguzi wa rais wa Nigeria anajua vyema kuwa anakabiliwa
na upinzani mkali kutoka kwa Muhammadu Buhari. Katika mazingira kama
hayo, iwapo jeshi la kieneo litashindwa katika vita vyake dhidi ya Boko
Haram, basi suala hilo litachangia kwa kiasi kikubwa kushindwa mgombea
wa chama tawala katika uchaguzi huo.
0 comments:
Post a Comment