Sharti kuu la kufikia natija mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 ni kwamba makubaliano hayo yanapasa kujumuisha masuala yote wanayozusha hitilafu katika mjadala wa nyuklia; kwa msingi huo hakuna lolote litakalofikiwa hadi pale pande zote zitakapokubaliana kuhusu masuala yote. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa makubaliano kama hayo yanashabihiana na chemsha bongo ambayo ili kukamilika, vipande au sehemu zake zote zinapaswa kuunganishwa pamoja. Hata hivyo Zarif anaamini kuwa, nukta yenye umuhimu zaidi kwa ajili ya kufikiwa makubaliano ni maamuzi ya kisiasa ambayo yanapaswa kuchukuliwa. Zarif amesema, kuna watu wanaodhani kuwa matarajio na mustakbali wao wa kisiasa utadhaminiwa kwa kuendelea kuwepo hali ya machafuko, migogoro na mivutano, na maadamu hali hiyo itaendelea kuwapo basi suala la kuchukua maamuzi muhimu ya kisiasa litagubikwa na wingu zito.
Baadhi ya watu wanaopinga makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 linalojumuisha pamoja nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Ujerumani, miaka miwili iliyopita walikuwa wakisema kuwa, Iran haitaheshimu vipengee vya makubaliano ya Geneva. Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambaye yuko mstari wa mbele kati ya wapinzani hao Novemba mwaka 2013 alipinga vikali makubaliano ya Geneva na kuanzisha propaganda kubwa dhidi yake.
Tangu mwaka 1992 hadi sasa, Netanyahu amekuwa akidai kuwa, Iran itakuwa imeunda bomu la nyuklia katika kipindi cha miaka miwili, mitatu au minne. Akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2012, Netanyahu alidai kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja mwingine Iran itamikili silaha za nyuklia. Hata hivyo ripoti za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) moja baada ya nyingine zimethibitisha kuwa Iran imetekeleza ahadi zake zote kama ilivyotakiwa. Si hayo tu bali hata Shirika la Ujasusi la Israel (MOSSAD) pia limekadhibisha madai hayo ya Netanyahu. Vilevile miaka kadhaa iliyopita idara 16 za kiintelijensia za Marekani zilikanusha madai ya kuweko ukengeukaji wowote katika miradi ya nyuklia ya Iran.
Hayo yote yanaonyesha wazi namna Iran inavyoheshimu na kufungamana kikamilifu na ahadi zake. Pamoja na hayo Dakta Zarif amesema kuwa Iran iko tayari kuondoa wasiwasi uliopo kuhusu miradi yake ya kuzalisha nishati ya nyuklia japokuwa inaamini wasiwasi huo hauna msingi wana mashiko ya maana. Iran imetangaza mara kadhaa kwamba haina lengo la kuunda silaha za nyuklia na inaamini kuwa, kwa mujibu wa itikadi za kidini na kimaadili na vilevile katika fremu ya sera zake za kujilinda, kuunda na kutumia silaha za nyuklia ni marufuku na mwiko. Iran inaamini kuwa, silaha za nyuklia hazileti amani si kwa Iran wala nchi yoyote nyingine na inasisitiza kuwa maendeleo ya kielimu ni haki ya kila nchi na kwamba kutolewa madai yasiyo na msingi hakuwezi kukwamisha maendeleo ya elimu na sayansi ya kuzalisha nishati ya nyuklia.
0 comments:
Post a Comment