Huku ikikosoa hatua ya vyama vya
upinzani ya kususia uchaguzi huo, serikali ya Khartoum imesema kuwa
viongozi wa vyama hivyo hawafai kuiongoza nchi hiyo. Kwa kuongezeka
wimbi la upinzani nchini Sudan inaonekana kuwa hali ya mambo nchini humo
itakuwa ngumu zaidi kwa kuzingatia kukaribia kufanyika zeozi la
uchaguzi nchini. Awali chama tawala kilikuwa kimekiri kuwepo upinzani
kuhusiana na suala zima la
uchaguzi na hivyo kuitisha mazungumzo ya
kitaifa ili kujaribu kupunguza tofauti zilizopo kuhusu suala hilo. Hii
ni katika hali ambayo hadi sasa hakuna hatua yoyote ya maana
iliyochukuliwa kwa lengo la kutuliza hali ya mambo nchini, bali kinyume
chake serikali imekuwa ikikamata na kuwatia mbaroni viongozi wa upinzani
na hivyo kukiuka misingi ya demokrasia na vilevile kuvuraga zaidi hali
ya mambo nchini. Ni kutokana na suala hilo ndipo baadhi ya wataalamu wa
mambo wakasema kuwa hali hiyo huenda ikaharibu zaidi hali ya mambo
nchini Sudan hasa katika kipindi hiki nyeti cha kukaribia uchaguzi
mkuu.Wataalamu hao wanasema kuwa mashindano ya uchaguzi kati ya Rais
Omar al-Bashir na wapinzani si ya kiadilifu hata kidogo. Katika hali
ambayo rais huyo anatumia mali na vyombo vya habari vya umma kwa lengo
la kuendeshea kampeni zake za uchaguzi, wapinzani wamenyimwa haki hiyo.
Katika upande wa pili marekebisho
yaliyofanyika katika katiba ya Sudan, yanampa Rais Bashir uwezo wa
kuwachagua magavana wa majimbo katika hali ambayo magavana hao wanapasa
kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi. Katika upande wa pili, uchaguzi
hautafanyika katika majimbo ya Darfur, Jabal an-Nuba na Blue Nile
kutokana na kuendelea mapigano katika majimbo hayo. Kutokuwepo vyombo
huru vya mahakama nchini Sudan ni jambo jingine ambalo limezidisha
mivutano ya kisiasa nchini humo. Vyombo hivyo kwa sasa vinadhibitiwa
kikamilifu na serikali na rais ndiye aliye na uwezo wa kuwapa na
kuwafuta kazi majaji wa mahakamu kuu. Wanachama wa tume huru ya uchaguzi
pia wanateuliwa moja kwa moja na rais, jambo linalowafanya waogope
kumkosoa kwa njia yoyote ile. Wapinzani pia wanasema kuwa Rais Bashir
hafai kuiongoza nchi kutoka na kuwa anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya
Jinai ICC. Kushindwa serikali ya al-Bashir kuimarisha uchumi wa Sudan
ni sababu nyingine inayotolewa na wapinzani dhidi yake. Hivi sasa
viwanda vingi vya nchi hiyo vimefilisika na madeni yake ya nje
yanapindukia dola bilioni 40. Wapinzani pia wanaashiria kujitenga Sudan
Kusini na Sudan na tetesi za kujitenga maeneo mengine ya nchi hiyo
likiwemo jimbo la Darfur, kuwa miongoni mwa mambo yanayowafanya wadai
kuwa al-Bashir hana tena uwezo wa kuongoza nchi. Wataalamu wa mambo pia
wanaashiria kuenea ufisadi, rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma
unaofanywa na viongozi wa ngazi za juu serikalini kuwa baadhi ya mambo
ambayo yangemfanya Bashir ashindwe kwenye uchaguzi, kama uchaguzi huo
ungekuwa huru na wa haki.
0 comments:
Post a Comment