
Rais Barack Obama wa Marekani amesema anaamini kwamba makubaliano
ya nyuklia kati ya Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1 yameandaa
mazingira ya kuboreshwa uhusiano kati ya Washington na Tehran.
Akizungumza juzi Jumamosi katika mahojiano aliyofanyiwa na kanali ya
televisheni ya CNN, Obama alisema makubaliano ya nyuklia yanaandaa
mazingira ya kufikiwa lengo kuu ambalo ni kuboreshwa uhusiano baina ya
Washington na Tehran.
Hadi sasa, Marekani imepoteza fursa nyingi za kuboresha uhusiano na
Iran; hivyo kuzungumzia maelewano ya siku za usoni kati ya Marekani na
Iran, hata kama ni kwa kwango cha utoaji kauli tu kungali mbali mno na
uhalisia wa mambo. Masuala mengi machungu bado yangaliko ambayo wingu
lake jeusi lingali limetanda kwa miaka na miaka sasa kwenye anga ya
uhusiano wa Iran na Marekani. Obama anadai kwamba nia yake si kuwa na
uadui na Iran, lakini katika kutetea kwake makubaliano ya nyuklia angali
ameshikilia madai kuwa Iran ni tishio, na kwamba hatua ijayo
atakayochukua katika Mashariki ya Kati ni kupunguza kile alichodai,
wasiwasi unaotokana na siasa za Iran katika eneo hili. Marekani inawapa
ahadi waitifaki wake wa jadi na majirani wa Iran kuwa itaendelea
kuwauzia silaha za mabilioni ya dola ili eti kuwafanya wawe imara
kukabiliana na vitisho vya Iran, hatua ambayo ni ya kuchochea mifarakano
kati ya nchi za eneo na kueneza sumu ya hali ya kutoaminiana baina yao.
Katika sehemu nyengine ya mahojiano hayo aliyofanyiwa na CNN, Rais wa
Marekani alisema pia kama ninavyomnukuu:”Sisi tumefanya mazungumzo na
utawala unaopiga nara za ‘mauti kwa Marekani’; hata hivyo hakusema ni
kwa nini wananchi wa Iran wanapiga nara na sha’ar hizo. Ili kuelewa
chanzo na sababu ya hatua za kiadui za Marekani dhidi ya Iran, inafaa
tuuangazie mwenendo wa Washington, si katika kipindi cha miongo mitatu
tu nyuma, bali kwa kipindi chote cha nusu karne iliyopita. Hatua za
kiadui za Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hazijakomea
kwenye mapinduzi ya kijeshi au vitendo vya ujasusi tu vilivyokuwa
vikifanywa na ubalozi wa nchi hiyo hapa mjini Tehran. Katika hatua yake
ya kwanza mara baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Marekani
ilichukua uamuzi wa kiadui kwa kuzuia fedha na mali za Iran zilizokuweko
katika mabenki ya nchi hiyo na hivyo kuanzisha rasmi kampeni ya
kuliwekea mzingiro wa kiuchumi taifa hili na kutaka litengwe; na katika
kipindi cha miaka yote iliyopita baada ya hapo imechukua hatua kadha wa
kadha kwa lengo la kuvuruga uthabiti ndani ya Iran. Jaribio la uvamizi
wa kijeshi la mwezi Aprili mwaka 1981 katika jangwa la Tabas mashariki
mwa Iran na kuuunga mkono utawala wa Saddam katika vita vya miaka minane
ulivyoanzisha dhidi ya Iran, yote hayo yalifanyika kwa lengo hilo.
Shambulio la mwezi Julai mwaka 1988 la kombora la manuwari ya Marekani
ya USS Vincennes, lililoitungua kwa makusudi ndege ya abiria ya Iran ni
jinai nyengine iliyofanywa na Washington na kusababisha vifo vya abiria
290 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo iliyokuwa ikitoka Bandar Abbas
kuelekea Dubai. Misimamo na harakati zote hizo za kiadui ni kumbukumbu
za faili chafu la nusu karne ya uingiliaji na uadui wa Marekani dhidi ya
taifa la Iran, kumbukumbu ambazo haziwezi kufutika katu ndani ya fikra
za Wairani na historia ya nchi yao. Japokuwa hivi sasa Obama anajaribu
kuonyesha kuwa mwenendo wake yeye ni tofauti na watangulizi wake, lakini
kivitendo amethibitisha kuwa mtazamo wake juu ya Iran hauna tofauti ya
kiasi hicho kulinganisha na waliomtangulia. Ndiyo kusema kuwa dhana na
utabiri juu ya uhusiano wa Marekani na Iran baada ya makubaliano ya
nyuklia unategemea mambo mengi ambayo wakati ndio utakaohukumu juu yake.
Na kwa hivyo katika kipindi hiki cha sasa mazungumzo kati ya Iran na
Marekani yamefanyika kuhusiana na kadhia ya nyuklia tu, si zaidi ya
hilo. Na mtazamo wa Iran juu ya Marekani utaweza kubadilika pale
yatakaposhuhudiwa mabadiliko ya kweli katika mwenendo na muamala wa
Washington…/
0 comments:
Post a Comment