KOCHA wa Yanga, Hans Pluijm, ametamka kwamba amepata karibu kila kitu kuhusu wapinzani wao wa Kombe la Shirikisho, BDF XI ya Botswana na hapohapo akatamka staili moja muhimu watakayoitumia kuwaumiza wanajeshi hao kuwa ni kasi ya kutosha kwa viungo wake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Pluijm alisema amepata
marafiki zake wengi kutoka Afrika Kusini ambao wamemsaidia kupata mbinu
za kuwaumiza BDF XI kwa kumpatia mkanda mmoja wa video ya mechi za timu
hiyo ambao wamemtaka kutumia viungo wenye kasi kuwachosha wanajeshi hao.
Katika kujipanga na hilo, Pluijm ameanza mikakati
ya kuwapa kazi viungo; Simon Msuva, Mrisho Ngassa na Andrey Coutinho
kuwachosha BDF XI kwa kufungua uwanja.
Pluijm alisema kasi ndiyo silaha pekee ambayo
itawasaidia kuwaumiza wapinzani wao hao ambao zaidi ametahadharishwa
kwamba wanajeshi hao wapo vizuri kwa fiziki ingawa mabadiliko ya hali ya
hewa yanaweza kuwaathiri.
Alisema Botswana haina tofauti kubwa na Afrika
Kusini ambao wamekuwa na hali ya hewa ya baridi na hivyo watapata tabu
kidogo kutokana na joto la Dar es Salaam.
“Nimepata kila kitu, kwa sasa la muhimu ni
kuangalia maandalizi yetu, naweza kusema tupo tayari kwa vita na hao
wanajeshi,” alisema Pluijm.
“Nimeambiwa kwamba tunatakiwa kutumia kasi
kuwaumiza hawa jamaa na hilo hatuna shaka nalo kwa kuwa watu wa
kutufanyia kazi hiyo tunao katika timu yetu, mtu kama Simon (Msuva) na
Ngassa (Mrisho) ni watu mwafaka kwa hilo.”
Yanga itaumana na BDF kesho Jumamosi Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
CANNAVARO
Katika hatua nyingine, Pluijm ametamka kwamba
licha ya matarajio makubwa aliyonayo nahodha wake Nadir Haroub
‘Cannavaro’ ndiye mtu pekee anayemchanganya.
Pluijm alisema Cannavaro amezua hofu katika kambi
yao kufuatia kupata maumivu ya goti la kulia ambapo bado haijajulikana
juu ya majaliwa yake.
Pluijm alisema Cannavaro atalazimika kusubiri kwa
siku mbili kuanzia jana kujua hatma yake kama atakuwa tayari kwa mchezo
huo wa kwanza baina ya timu hizo.
0 comments:
Post a Comment