
Waziri Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph Warioba
amevitaka vyama vya siasa nchini humo kuzingatia matakwa ya wananchi
katika suala zima la Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa badala ya
kuwagawa. Warioba amesema anaamini kwamba, baadhi ya vipengele
vilivyokataliwa katika Rasimu ya Katiba, ipo siku vitafanyiwa kazi
kuondoa migongano huku akisisitiza, kisheria kura ya maoni siyo mwisho
wa mchakato. Waziri Mkuu huyo mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
amesema kuwa, kwa sasa, badala ya kuwaweka wananchi pamoja na
kukubaliana wanachotaka , upo mvutano huku wengine wakitaka Katiba
Iliyopendekezwa ikubaliwe na wengine wakitaka wananchi waikatae. Hayo
yanajiri katika hali ambayo mrengo wa upinzani nchini Tanzania chini ya
mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) umetangaza kutoshiriki
katika kura ijayo ya maoni ya Katiba. Aidha akihutubia mkutano wa
hadhara hivi karibuni huko Zanzibar, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi
(CUF) Maalim Seif Sharif Hamad alitangaza rasmi kwamba, chama chake
hakitashiriki katika kura hiyo ya maoni ya Katiba iliyopendekezwa
kutokana na kupuuzwa matakwa ya wananchi.
0 comments:
Post a Comment