Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ameandaa muswada wa kuuwasilisha
bungeni wenye lengo la kufanyiwa marekebisho ya kimsingi sheria ya
kumiliki ardhi nchini humo. Taarifa kutoka Pretoria zinasema kuwa,
mpango huo wa Rais Zuma utawazuia raia wa kigeni kumiliki ardhi nchini
humo. Kwa mujibu wa mpango huo, wazalendo wa Afrika Kusini wataweza
kumiliki ardhi isiyozidi ukubwa wa hekta elfu kumi na mbili na wageni
wote hawataruhusiwa kumiliki ardhi, bali watakodishwa kwa muda wa kati
ya miaka 30 hadi 50. Hatua ya Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ina
mwelekeo wa kupata uungaji mkono kutoka kwa wazalendo wausi walio wengi
nchini humo, na hasa ikizingatiwa kuwa utajiri mkubwa wa nchi hiyo
unamilikiwa na wageni. Nchi za Kiafrika zinakabiliwa na migogoro mingi
ya umiliki wa ardhi, kutokana na matajiri na wageni kujilimbikizia
maeneo makubwa ya ardhi huku wenyeji wakiambulia sehemu ndogo tu ya
ardhi zisizo na rutuba kwa shughuli za kilimo na ufugaji. Inafaa
kuashiria hapa kuwa, miaka ya hivi karibuni Zimbabwe ilitumbukia kwenye
mgogoro mkubwa na nchi za magharibi, baada ya Rais Robert Mugabe wa nchi
hiyo kuwanyang'anya wageni mashamba makubwa waliyokuwa wakiyamiliki na
badala yake kuwapatia maveterani wa vita na wazalendo wa nchi hiyo,
suala lililokabiliwa na upinzani mkubwa kutoka nchi za Magharibi.
0 comments:
Post a Comment