
Wataalamu wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa IMF wamesema kuwa,
Zimbabwe itakabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi katika mwaka huu wa 2015.
Kwa kuzingatia ukuaji duni wa kiuchumi nchini Zimbabwe sambamba na
madeni mengi yanayoikaba koo nchi hiyo, basi yamkini nchi hiyo ya kusini
mwa Afrika ikakabiliwa na matatizo mengi. Domenico Fanizza, Mkuu wa
Kamati ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa IMF iliyotumwa Harare Zimbabwe
amesema hayo katika safari yake nchini humo. Lengo la safari hiyo
limetajwa kuwa ni kuchunguza ukuaji wa uchumi pamoja na uwazi kuhusiana
na kiwango cha madeni ya nchi hiyo. Licha ya kushuka bei ya mafuta
katika soko la dunia, wataalamu wa mambo wanatabiri kwamba, uchumi wa
Zimbabwe utazidi kulegalega mwaka huu. Ni karibu muongo mmoja sasa
ambapo uchumi wa Zimbabwe umedorora kutokana na kiwango cha juu cha
ukosefu wa ajira na ukuaji wa kusuasua wa uchumi wa nchi hiyo. Baadhi ya
wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, sera mbovu za kiuchumi za serikali
ya Harare katika miongo ya hivi karibuni ndizo zilizoufanya uchumi wa
nchi hiyo kukabiliwa na hali mbaya. Rais Robert Mugabe mwaka 2000
alianza kutekeleza mpango wa marekebisho ya ardhi katika maeneo yote ya
nchi hiyo. Lengo la mpango huo lilikuwa ni kupora ardhi bora kwa kilimo
za wazungu na kuzigawa baina ya wazalendo masikini wa nchi hiyo. Sera za
Rais Mugabe za kukabiliana na wakoloni wa zamani wa Ulaya kama
Uingereza zimemfanya aendelee kubakia madarakani kutokana na himaya na
uungaji mkono wa wazalendo weusi wa nchi hiyo katika kila chaguzi. Sera
hizo za Mugabe zimekuwa zikiwavutia wapiga kura wazalendo weusi ambao
ndio wanaounda asilimia kubwa ya wakazi wa nchi hiyo ya kusini mwa
Afrika. Pamoja na hayo, utumiaji mabavu wa wafuasi wenye misimamo mikali
wa chama tawala cha ZANU-PF katika kupora ardhi na kuwauwa wamiliki
weupe wa ardhi kuliitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro ambapo hadi sasa
athari mbaya za mgogoro huo zingali zinashuhudiwa. Katika upande
mwinginme, kufukuzwa wazungu elfu nne katika ardhi walizokuwa
wakizimikili na kisha ardhi hizo kugawia wazalendo weusi wa nchi hiyo,
kulipelekea wazungu wengi waliowachache kuikimbia nchi hiyo. Kutokuwa na
tajiriba wazalendo weusi wa Zimbabwe katika masuala ya kilimo na kukosa
vyanzo vya fedha kuliifanya sekta ya kilimo Zimbabwe idorore katika
kipindi cha muda mfupi. Kuadimika bidhaa za mazao kama mahindi nchini
Zimbabwe, nchi ambayo katika kipindi fulani ilikuwa mashuhuri kwa jina
la “Kikapu cha Mkate Afrika” kwa maaana ya mzalishaji mkubwa wa chakula
barani Afrika kuliufanya uchumi wa nchi hiyo uzidi kudidimia. Hata kama
Rais Mugabe na viongozi wa chama tawala cha ZANU-PF hawakuwa tayari
kukiri kushindwa mpango wa marekebisho wa ardhi, lakini hatimaye tarehe
27 Februari mwaka huu, kiongozi huyo wa Zimbabwe alikiri kwamba, sera za
ardhi hazikuwa sahihi. Pamoja na hayo, juma lililopita, Rais Mugabe
aliwaonya wakulima weupe kwamba, atawapokonya ardhi wanazomiliki. Weledi
wa masuala ya kiuchumi wanaamini kuwa, kukabidhiwa mashamba wazalendo
weusi wa Zimbabwe ambao hawakuwa na ustadi katika masuala ya kilimo
kulitoa pigo kubwa kwa sekta ya uchumi wa nchi hiyo.
0 comments:
Post a Comment