Weledi wa mambo wanaamini kuwa, kuendelea harakati za Boko
Haram katika hali ya hivi sasa nchini Nigeria ni kwa maslahi ya baadhi
ya serikali na ni kwa sababu hii ndio nchi kama Marekani, huku
zikijionyesha kama wapinzani wa ugaidi, zikaandaa mazingira ya
kuendelea harakati za kundi hilo la kigaidi.
Kwa kuzingatia uwezo mkubwa walionao magaidi wa Boko Haram
hasa kwa mtazamo wa wapiganaji, zana za kivita na uwezo wa kiufundi na
kilojistiki ni wazi kuwa Boko Haram wanapata himaya ya kigeni kwa
malengo maalumu. Kuidhoofisha serikali ya Nigeria kama dola lenye nguvu
Afrika na kuifanya ishughulike tu na mgogoro wa ndani ya nchi ni moja
kati ya malengo ya Marekani. Hivi sasa gharama za kijeshi na kiusalama
zimechukua sehemu kubwa ya bajeti ya Nigeria. Hii ni katika hali ambayo
aghalabu ya watu wa Nigeria wanaishi kwa pato la chini ya dola mbili kwa
siku katika hali ambayo nchi hiyo ina utajiri mkubwa sana wa mafuta na
gesi. Katika upande mwingine, ukosefu wa usalama na mgogoro wa ndani ya
Nigeria unaongozwa kwa njia maalumu ili kuhakikisha sekta za mafuta na
gesi nchini humo haziathiriki. Hii ndio sababu tunashuhudia hujuma za
Boko Haram zikiwa katika eneo la Kaskazini mwa Nigeria na si eneo la
kusini lenye utajiri wa mafuta. Sababu ya jambo hili ni kuhifadhi vyanzo
vya nishati Nigeria ili mbali na Marekani , nchi za Ulaya ziendelee
kupora utajiri wa nchi hiyo huku serikali ya nchi hiyo ikijishughulisha
na mgogoro wa ndani.
Kuendelea harakati za Boko Haram pia kuna umuhimu mwingine
kwa nchi za Magharibi. Kuenea fikra potofu za Boko Haram bila shaka
kutapelekea kuchafuliwa sura ya Waislamu na Uislamu duniani. Nukta hii
ni muhimu kwa vyombo vya habari na watawala wa nchi za Magharibi ambao
wanataka kuendeleza sera zao za chuki dhidi ya Uislamu. Kuathiri
mchakato wa uchaguzi nchini Nigeria ni lengo jingine la madola ya
kibeberu katika kuunga mkono kwa njia isiyo ya moja kwa moja ugaidi wa
Boko Haram. Uchaguzi wa rais nchini Nigeria unatazamiwa kufanyika katika
kipindi cha wiki chache zijazo. Kwa hivyo kuibua vita na machafuko
katika maeneo ya kaskazini yenye wakaazi wengi Waislamu hasa eneo la
Kaskazini Mashariki kutapelekea Waislamu wapate matatizo katika upigaji
kura na yamkini wasiweze kumpigia kura mgombea wanayemtaka. Nchi za
Magharibi zinatumai kuwa, kuchaguliwa tena rais Mkristo nchini Nigeria
kutavunja ile desturi ya kubadilishana uongozi baina ya Mwislamu na
Mkristo katika nchi hiyo kubwa ya Magharibi mwa Afrika. Rais wa sasa wa
Nigeria, Goodluck Jonathan ni Mkristo kutoka eneo lenye utajiri wa
mafuta la Kusini. Kwa mujibu wa sheria ambayo haijaandikwa Nigeria,
baada ya kumalizika muhula wa kisheria wa rais Mkristo rais anayefuata
anapaswa kuwa Mwislamu.
0 comments:
Post a Comment