 
     
    Viongozi mbalimbali wa Tanzania 
wameendelea kutuma salamu za rambirambi kufuatia msiba mkubwa 
uliolikumba taifa hilo la Afrika Mashariki baada ya watu wasiopungua 42 
kufariki dunia katika ajali ya barabarani hapo jana mkoani Iringa. Rais 
Jakaya Kikwete amewaongoza Watanzania kuomboleza vifo vya raia wenzao 
waliopoteza maisha baada ya kutokea ajali mbaya ya barabarani. Rais 
Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, 
na kuwahakikishia wafiwa wote kuwa yuko pamoja nao na kuwaombea majeruhi
 wote wapone haraka ili waendelee na shughuli zao za ujenzi wa taifa. 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bi Amina Masenza amesema katika salamu zake za 
rambirambi kama ninavyomnukuu: “msiba huu ni wa watu wote, siyo wa mtu 
mmoja, nimesikitika sana kusikia kuwa asubuhi kuna ajali ilitokea  eneo 
la Changarawe nje kidogo ya mji wa Mafinga, na niliposikia nimekuja mara
 moja kuangalia ni jinsi gani tutafanya ili kuwasaidia ndugu hawa.” 
Zaidi ya watu 42 walipoteza maisha katika ajali hiyo ya jana huko 
Mafinga Mkoani Iringa. Ajali hiyo ilihusisha lori la mizigo na basi la 
abiria ambalo kufuatia ajali hiyo liliangukiwa na Kontena na 
kulikandamiza.
 
    
0 comments:
Post a Comment