
Idadi ya wakimbizi wa Burundi
waliokimbilia nchi jirani kufuatia ghasia zinazoendelea nchini mwao
imeongezeka na kufikia elfu hamsini katika wiki moja iliyopita pekee.
Hiyo ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi
(UNHCR) ambalo limesema raia hao wamekimbilia Rwanda, Tanzania na
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Idadi kubwa ya wakimbizi wamekimbilia
Rwanda na sasa Tanzania baada ya vizuizi vya kuingia kuondolewa na wengi
wao ni wanawake na watoto wakikumbwa na madhila. Adrian Edwards,
msemaji wa UNHCR, Geneva amesema kuwawanawake wengi wameripoti kubakwa
na watu wenye silaha, mbali na madhila mengine, wakihonga ili waweze
kupita kwenye vizuizi barabarani huku wengine wakitembea saa nyingi
porini wakiwa na watoto wao. UNHCR imetoa wito kwa mamlaka za Burundi
kuruhusu watu watembee kwa uhuru, na muhimu mipaka ikabakia wazi.
Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita
Burundi imekumbwa na machafuko na ghasia kufuatia tangazo la Rais
Pierre Nkurunziza kuwa atawania urais kwa muhula wa tatu. Takribani watu
15 wamepoteza maisha katika ghasia hizo. Wapinzani wanasema Nkurunziza
anakiuka Mapatano ya Arusha yaliyomaliza vita vya ndani nchini humo,
lakini wafuasi wa rais huyo wanasema katika muhula wake wa kwanza
Nkurunziza alichaguliwa na Bunge na hivyo muhula huo hauwezi kuhesabiwa.
0 comments:
Post a Comment