Uchaguzi mkuu wa rais wa Ivory Coast umepangwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu na tayari shughuli ya kujiandikisha wagombea wa urais ilianza jana Jumatatu. Uchaguzi ujao huko Kodivaa unafuatiliwa kwa karibu hasa ikizingatiwa kuwa, uchaguzi uliopita wa mwaka 2010 ulikumbwa na ghasia na machafuko baada ya Laurent Gbagbo, rais wa wakati huo kukataa matokeo ya uchaguzi baada ya kupigwa mweleka na mpinzani wake, Alassane Ouattara.
Wafuatiliaji wa siasa za Ivory Coast wanatofautiana kuhusu tathmini ya nani atashinda uchaguzi wa mwaka huu kutokana na kuchelewa kambi ya upinzani kumtaja mgombea mmoja atakayechuana na rais wa sasa. Chama tawala cha RDR kimeshatangaza kuwa, Rais Ouattara ndiye atakayepeperusha bendera kwenye kinyang'annyiro cha Oktoba. Kiongozi huyo amepata uungaji mkono wa baadhi ya viongozi wa vyama vingine kama vile chama cha PDCI kinachoongozwa na Henri Konan Bédié. Ingawa Bédié amewataka wafuasi wa chama chake wamuunge mkono Ouattara kwenye uchaguzi mkuu ujao, kauli hiyo imepingwa vikali na wanachama wengine wa PDCI ambao wamesisitiza kuwa chama hicho kitamsimamisha mgombea wa urais kwenye uchaguzi huo wa Oktoba; jambo linaloashiria mpasuko ndani ya chama hicho. Katika uchaguzi uliopita mpasuko kama huo pia ulishuhudiwa na matokeo yake yakawa ni kumsafishia njia Bw. Ouattara kushinda kiti cha rais. Kiongozi huyo safari hii pia anatarajiwa kunufaika na vuta nikuvute iliyoko kwenye chama hicho kujipatia ushindi.
Uchunguzi unaonyesha kuwa, umaarufu wa Rais Alassane Ouattara umeshuka mno katika miaka ya hivi karibuni na wajuzi wa mambo wanasema hilo limetokana na kuendelea kuongezeka umasikini, kupanda maradufu bei za bidhaa muhimu, kuendelea kudorora sekta za afya na elimu katika kipindi cha kwanza cha utawala wake. Wadadisi wanasema mambo hayo yanaweza kuwa kikwazo kwa Rais Ouattara kushinda tena kipindi kingine kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment