Viongozi wa Ufaransa na Ujerumani wamesema wameridhishwa kuona kwamba usitishwaji wa mapigano mashariki mwa Ukraine unafuatiliwa kwa kina.
Mashuhuda wanasema katika maeneo mengi kuna utulivu, tofauti na mji wa Debaltseve ambapo makundi ya waasi wanaoungwa mkono na Urusi wameendelea kushambulia vikundi vya serikali walivyovizunguka katika eneo la usafiri.
Hata hivyo, mapigano yamepungua tofauti na ilivyokuwa hapo Jumapili. Kundi la usalama la ulaya limesema waasi wamewazuia waangalizi wa kundi hilo, na kusema kwamba makubaliano ya amani yameanza kuzaa matunda.
Msemaji wa jeshi wa Ukraine, Andriy Lysenko - amesema wakazi wa mashariki mwa Ukraine wamethibitisha kwamba mapigano yamepungua.
"Hali mashariki mwa Ukraine inaelekea kuimarika. Wakazi wa maeneo ya Donetsk na Luhansk, kupitia mitandao ya kijamii wamethibitisha kuwepo kwa hali ya utulivu nje ya nyumba zao. Hata hivyo, licha ya kuwepo kwa usitishwaji wa mapigano, bado milio ya silaha inasikika mara moja moja. Kuanzia mwanzo wa usitishwaji wa mapigano, magaidi wameshambulia mara kumi upande wetu kwa kutumia mabomu ya kutupa kwa mkono.")
Nae waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Pavlo Klimkin amesema wakati hali ikiendelea kuimarika, Kiev inafuatilia kwa karibu hali hiyo. "Haya ndio baadhi ya matukio ya ukiukwaji wa usitishwaji wa mapigano tulioushuhudia. Hali imeimarika ikilinganishwa na siku chache zilizopita. Sharti tuiangalie hali hiyo na kufanya kila tuwezalo dhidi ya wale wanaokiuka masharti. Hali ikizidi kuwa mbaya, basi tutatafuta njia ya kuchukua hatua."
0 comments:
Post a Comment