Leo ni Jumapili tarehe 25 Mfunguo Saba Rabiu th-Thani mwaka 1436 Hijria, sawa na tarehe 15 Februari mwaka 2015 Miladia.
Siku kama ya leo, miaka 1148 iliyopita,
alifariki dunia Al-Ṣabi Thābit ibn Qurra, mtaalamu wa hesabati, mnajimu
na tabibu wa kipindi cha utawala wa Abbasiya. Ibn Qurra alizaliwa mwaka
221 Hijiria, mjini Harran, Iraq, na kujifunza lugha za Kigiriki, Syriac
na Kiarabu. Baadaye msomi huyo alielekea mjini Baghdad kwa ajili ya
kujiendeleza zaidi kimasomo ambapo alitokea kuwa mtaalamu mkubwa wa
hesabati na mnajimu mashuhuri wa Kiislamu.
*******
Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, Jeshi
Jekundu la Shirikisho la Urusi ya Zamani lililazimika kuondoka nchini
Afghanistan baada ya kuikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa miaka kumi.
Majeshi hayo yaliondoka baada ya kushindwa kukabiliana na muqawama wa
mujahidina wa Kiislamu. Lengo la Umoja wa Sovieti la kuivamia na
kuikalia kwa mabavu Afghanistan mwaka 1979, lilikuwa ni kuizatiti na
kuitia nguvu serikali kibaraka ya Kabul iliyokuwa ikiungwa mkono na
Moscow na kueneza satua yake upande wa maeneo ya kusini mwa Asia. Hatua
hiyo iliyoyatumbukiza hatarini maslahi ya Marekani, ilikabiliwa na
radiamali kali ya Washington ambapo Ikulu ya Marekani (White House)
ilianzisha operesheni za kuyatoa majeshi ya Umoja wa Sovieti huko
Afghanistan. Hatimaye baada ya miaka 10 wananchi wa Afghanistan
wakisaidiwa na Mujahidina walifanikiwa kuhitimisha uvamizi huo na
kuyatoa majeshi ya Urusi katika ardhi yao.
*******
Miaka 233 iliyopita kwa mujibu wa kalenda
ya Miladia, vilianza vita vya majini kati ya Ufaransa na Uingereza
katika pwani ya India. Vita hivyo vilivyodumu kwa muda wa miezi saba,
vilikuwa ni mlolongo wa vita kati ya nchi mbili hizo vilivyokuwa na
lengo la kuikoloni India na kupora utajiri wake. Ijapokuwa Ufaransa
ilishinda vita hivyo, lakini nchi hiyo haikuweza kurejea India na
kuikoloni nchi hiyo, na badala yake Uingereza ilibaki na kuendelea kuwa
mkoloni mkuu huko Bara Hindi.
*******
Na siku kama ya leo miaka 207 iliyopita,
mfalme wa Urusi ya zamani aliidhibiti kikamilifu nchi ya Finland. Katika
karne 11 Miladia, Finland ambayo ilikuwa inakaribiana na dola kubwa la
Urusi ya Zamani na ilikuwa inahisi hatari kutoka kwa jirani huyo,
iliomba msaada kutoka kwa Sweden ambayo ilikuwa ikishindana na Urusi.
Suala hilo lilipelekea Sweden nayo kuidhibiti Finland katika karne ya 15
Miladia na baada ya kudhoofika Sweden na satwa kuchukuliwa ya Urusi,
sehemu kadhaa za Finland ziliangukia mikononi mwa Warusi na hatimaye
nchi hiyo ikadhibitiwa kikamilifu na Urusi ya Zamani kwenye siku kama ya
leo na baada ya kupita karibu miaka 650 ya kudhibitiwa na Sweden.
0 comments:
Post a Comment