Siku kama ya leo miaka 1431
iliyopita alizaliwa Bibi Zainab (s.a) binti mtukufu wa Imam Ali bin Abi
Twalib na Bibi Fatimatu Zahraa (as). Bibi Zainab alikuwa mashuhuri
miongoni mwa watu kutokana na maarifa na elimu kubwa aliyokuwa nayo.
Katika tukio la Karbala, Bibi Zainab (s.a) alisimama kidete na
kukabiliana na dhulma za watawala dhalimu na ujahili watu wa zama hizo
ili kutimiza malengo matukufu ya kaka yake, Imam Hussein (a.s). Bibi
Zainab alipelekwa Sham pamoja na mateka wengine wa Nyumba Tukufu ya
Mtume (saw) baada ya mapambano ya Imam Hussein (a.s) huko Karbala.
Hotuba za Bibi Zainab mbele ya majlisi ya Ibn Ziyad mtawala wa Kufa na
katika ikulu ya Yazid bin Muawiya huko Sham zilikuwa na taathira kubwa
katika kufichua dhulma na ukandamizaji wa Bani Umayya na kuonesha jinsi
Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume walivyodhulumiwa.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa nchini Iran siku ya kuzaliwa Bibi Zainab (a.s) husherehekewa kama 'Siku ya Wauguzi'.
Miaka 167 iliyopita katika
siku kama ya leo, utawala wa muda au duru ya pili ya utawala wa Jamhuri
nchini Ufaransa ilianza kufuatia mapambano yaliyoanzishwa na wananchi wa
Ufaransa na kujiuzulu Louis Philippe, mfalme dhalimu wa nchi hiyo.
Mfumo huo wa utawala unatajwa pia katika historia ya Ufaransa kwa jina
la utawala wa waandishi wa habari wa magazeti kutokana na kuwa,
waandishi wa habari kumi na moja wa magazeti wakiongozwa na Alfonso de
la Martin aliyekuwa malenga na mwandishi, ndio waliokuwa wakiongoza
utawala huo.
Na siku kama ya leo miaka 66
iliyopita, ulitiwa saini mkataba wa kuacha mapigano kati ya wawakilishi
wa Misri na utawala wa Kizayuni wa Israel katika kisiwa cha Rhodes
katika bahari ya Aegean. Baada ya kuundwa dola haramu la Israel katika
ardhi ya Palestina hapo mwaka 1948, Misri pamoja na nchi nyingine za
Kiarabu, iliingia katika vita dhidi ya utawala huo bandia. Hata hivyo
jeshi la Israel lilishambulia vikosi vya Waarabu ambavyo havikuwa na
zana za kisasa za kivita na kuingia katika ardhi za Misri na Lebanon
baada ya kuvishinda vikosi hivyo. Vita hivyo vilimalizika Januari mwaka
1949 ambapo katika tarehe kama ya leo pande mbili zilitia saini mkataba
wa kuacha vita chini ya upatanishi wa Umoja wa Mataifa. Nchi nyingine za
Kiarabu pia zikaukubali mkataba huo. Kwa mujibu wa mkataba huo eneo la
Ukanda wa Gaza liliwekwa chini ya mamlaka ya Misri.
0 comments:
Post a Comment