Leo ni Jumatano tarehe 28 Rabiuthani 1436 sawa na 18 Februari 2015.
Siku kama ya leo miaka 50
iliyopita nchi ya Gambia ilifanikiwa kupata uhuru kutoka kwa mkoloni
Mwingereza. Gambia ilikuwa koloni la kwanza la Uingereza barani Afrika.
Uingereza iliikoloni nchi hiyo mwaka 1588 na kuendelea kupora maliasili
za nchi hiyo kwa karibu karne nne. Mwaka 1963 Uingereza ambayo
ilidhoofika kisiasa na kiuchumi kutokana na athari za Vita vya Pili vya
Dunia haikuwa tena na uwezo wa kuendelelea kuikoloni Gambia na nchi hiyo
ikapata utawala wa ndani. Mwaka 1965 katika siku kama ya leo Gambia
ilijipatia uhuru wake.
Siku kama ya leo miaka 181
iliyopita sawa na tarehe 18 Februari mwaka 1834 vikosi vya majeshi ya
Ufaransa ambavyo vilianza kuikalia kwa mabavu Algeria mwaka 1830,
vilishindwa vibaya na wapiganaji wa Amir Abdulqadir Al Jazairi.
Kushindwa huko kulipelekea theluthi moja ya askari wa Ufaransa kuuawa na
nusu ya waliobakia kukamatwa mateka. Baada ya Wafaransa kushindwa
vibaya kwa mara ya kwanza barani Afrika, nchi hiyo ililazimika kusalimu
amri na kuomba yafanyike makubaliano ya amani. Hata hivyo Amir
Abdulqadir Jazairi alikataa ombi hilo hadi baada ya miaka miwili
iliyofuata, ambapo alifanikiwa kukomboa karibu ardhi yote ya Algeria
kutoka katika mikono ya Wafaransa.
Na miaka 798 iliyopita katika
siku sawa na ya leo Abubakar Muhyiddin Muhammad mashuhuri kwa jina la
Ibn Arabi, arif na msomi mkubwa wa Kiislamu aliaga dunia huko Damascus.
Alizaliwa mwaka 560 Hijria huko Andalusia, Uhispania ya leo. Ibn Arabi
alifanya safari nyingi katika baadhi ya nchi na miji ikiwemo Tunisia,
Makka na Baghdad na kila alipofika aliheshimiwa na kukirimiwa. Alikuwa
msomi hodari na baadhi ya duru zinasema kuwa ameandika vitabu na risala
zaidi ya 500. Miongoni mwa kazi zake kubwa ni vitabu vya "Tafsir Kabir",
"al Futuhatul Makkiyyah" na "Fususul Hikam".
0 comments:
Post a Comment