SIMBA itacheza na Polisi MoroLeoJumapili kwenye Uwanja wa
Jamhuri mjini Morogoro na kocha Goran Kopunovic amesema ni lazima
waibuke na ushindi ili kujiweka pazuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Kama ikishinda mchezo huo, timu yake hiyo inaweza kupanda hadi nafasi ya tatu.
Wakati Simba ikijiandaa na mchezo huo aliyekuwa
kocha wao Mserbia Zdravko Logarusic amepewa ulaji mpya na sasa atainoa
timu ya AFC Leopards ya Kenya.
Kocha huyo aliyetimuliwa na nafasi yake
kukabidhiwa Mzambia Patrick Phiri ambaye naye ametimuliwa, jana alisaini
mkataba wa miaka miwili na timu hiyo ya Kenya mbele ya Katibu Mkuu wa
Leopards, George Aladwa na ataanza kuinoa timu hiyo wiki ijayo.
Akizungumzia mechi ya Jumapili kocha wa sasa wa
Simba, Kopunovic alisema haijalishi anacheza kiwanja gani kwani aina ya
soka analotaka vijana wake wacheze ni la kushambulia na kusaka ushindi
kwa udi na uvumba na ndivyo itakavyokuwa katika mchezo huo na Polisi.
Kocha huyo wa zamani wa Polisi Rwanda alisema
anatarajia kufanya mabadiliko machache kuhakikisha wanaibuka na ushindi
mnono katika mechi hiyo ili kujiweka nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi
unaoongozwa na Azam yenye pointi 25 sawa na Yanga inayoshika nafasi ya
pili. “Napenda soka la kushambulia, hilo ndilo tutakalocheza keshokutwa
(leo) Jumapili dhidi ya Polisi, hayo ndiyo maandalizi niliyowapatia
wachezaji wangu,’’ alisema. “Sipendi kufanya mabadiliko mengi, tunaweza
kuwa na mabadiliko machache kutoka kikosi kilichocheza na Coastal Union,
labda moja ama mawili.”
Hata hivyo, Simba inaingia katika mchezo huo ikiwa
inafasi ya tisa na pointi 17 baada ya kucheza michezo 13 na kushinda
mitatu tu. Polisi wao wako nafasi ya tatu wakiwa na pointi 19 baada ya
kucheza mechi 14 na kushinda nne pekee. Mechi ya mwisho iliyozikutanisha
timu hizo ilimalizika kwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.
Kocha wa Polisi Moro, Adolf Rishard alisema:
“Tunafahamu kuwa tunakwenda kucheza na moja ya timu bora, mchezo wa
Jumapili hautakuwa rahisi kwani si Simba ile tuliyocheza nayo kwenye
mechi za mzunguko wa kwanza.”
Mechi nyingine inayochezwa jana Jumamosi ni kati
ya Coastal Union na Mbeya City kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga. Coasta iliingia uwanjani ikiwa nafasi ya saba na pointi 18 baada ya kucheza
mechi 14 wakati Mbeya City wapo nafasi ya 10 na pointi 16 baada ya
kucheza mechi 13.
Mechi tatu za mwisho zilizozikutanisha timu hizo, Mbeya City imeshinda mara mbili huku mchezo mmoja ukimalizika kwa sare.
Kocha wa Coastal, James Nandwa alisema: “Tumefanya mazoezi ya kufunga kwa wiki nzima hasa baada ya kugundua tuna upungufu huo.’’
Ofisa Habari wa Mbeya City, Dismas Ten alisema:
“Kikosi kipo kwenye hali nzuri, hatuna majeruhi na tunatarajia kiungo
Steven Mazanda aliyekosa mchezo wa mwisho kutokana na kadi za njano
atarejea.’’
0 comments:
Post a Comment