YANGA jana Alhamisi ilikamata usukani wa Ligi Kuu Bara baada ya
kuifunga Prisons mabao 3-0 na kuwashusha mabingwa watetezi Azam FC ambao
jana walibanwa na Ruvu Shooting na kutoka sare ya bila kufungana.
Yanga ilikuwa ugenini katika Uwanja wa Sokoine,
Mbeya na kwa ushindi huo imefikisha pointi 28, Azam ambayo pia ilikuwa
ugenini katika Uwanja wa Mabatini, Pwani sasa ipo nyuma ya Yanga baada
ya kufikisha 26 huku timu zote hizo zikiwa zimecheza mechi 14, mechi za
jana zilikuwa ni kiporo kwa timu zote.
Ushindi huo kwa Yanga ni mwendelezo mzuri wa mechi
zao za ligi ambapo keshokutwa Jumapili watacheza na Mbeya City katika
uwanja huo huo na wiki ijayo wataifuata BDF XI ya Botswana katika mechi
ya marudiano ya Kombe la Shirikisho. Wiki iliyopita Yanga iliifunga BDF
2-0 katika mechi ya kwanza iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga walianza mashambulizi ya maana mapema na kupata mabao mawili ya kuongoza ndani ya dakika 11 ikianza na la Simon Msuva.
Msuva alifunga dakika ya 3 akiunganisha vizuri
kona ya Andrey Coutinho na kuwaamsha vitini mashabiki wa Yanga. Coutinho
aliandika bao la pili dakika ya 11 baada ya shuti lake lililokuwa
likielekea wavuni kusindikizwa na beki wa Prisons, Lugano Mwangama.
Awali mpira huo ulianzia kwa shuti la Amisi Tambwe ambalo liliokolewa na
kipa wa Prisons, Mohammed Yusuph kabla ya kumkuta Coutinho aliyefumua
shuti lililomaliziwa na Lugano.
Msuva alihitimisha mabao ya Yanga dakika ya 55 alipounganisha kwa kichwa kona iliyopigwa na Coutinho.
Jacob Mwakalobo na Jeremiah Juma walishindwa
kuipatia mabao Prisons dakika za tisa na 10 baada ya mipira yao
kuokolewa na kipa wa Yanga, Ally Mustafa ‘Barthez’.
Mechi hiyo ilionekana kuchezwa zaidi katikati
kuanzia dakika ya 20 hadi 40 wakati dakika tano za mwisho wa kipindi cha
kwanza Mrisho Ngassa na Msuva walikosa nafasi ya kufunga baada ya
kushindwa kuelewana.
Yanga ilijikuta katika wakati mgumu baada ya
kiungo wake, Haruna Niyonzima kuumia baada ya kukanyagwa nyonga na Fred
Chudu lakini alilazimika kucheza huku akiwa anachechemea kwa kuwa Yanga
ilikuwa imemaliza idadi ya wachezaji wa akiba wanaopaswa kuingia.
Wakati huo huo Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles
Boniface Mkwassa ambaye pia aliwahi kuinoa Prisons na kuipa mafanikio,
amesema kwamba timu hiyo bado ina nafasi ya kujinasua isishuke daraja
kwani imeonyesha uwezo wa kutafuta nafasi lakini wameshindwa kuzitumia.
Wakati Yanga ikitakata Mbeya, Kocha wa Azam,
Joseph Omog aliamua kufanya mabadiliko katika kikosi kilichocheza na El
Merreikh ya Sudan katika Ligi ya Mabingwa.
Katika mabadiliko hayo wachezaji Kipre Bolou, Brian Majwega na Didier Kavumbagu hawakuwepo kikosi cha kwanza.
0 comments:
Post a Comment