Hivi sasa wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa wameunga mkono kikosi hicho kitakachobuniwa na nchi za Nigeria,
Cameroon, Chad, Niger na Benin. Iwapo rasimu iliyowasilishwa na nchi
tatu zilizotajwa itapasishwa na kuwa azimio katika Baraza la Usalama,
basi baraza hilo litaadhibu watu au nchi yoyote itakayounga mkono Boko
Haram. Lengo la kubuniwa kikosi hicho ambacho kitatekeleza majukumu yake
kwa mwaka mmoja litakuwa ni kurejesha amani katika mipaka ya nchi
jirani na Nigeria ambazo ni Chad, Cameroon, Niger na Benin. Kuenea kwa
vitendo vya uagaidi vya wanamgambo wa Boko Haram katika maeneo ya
kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuvuka mpaka hadi kwenye ardhi za
nchi jirani kama vile Niger na Chad kumewapelekea viongozi wa nchi hizo
wafikirie juu ya njia za kubuni kikosi cha kieneo cha kukabiliana na
magaidi hao wanaosababisha mauaji na hasara kubwa katika eneo. Tokea
mwezi Februari uliopita jeshi la Nigeria limekuwa likishirikiana na
askari wa Chad, Cameroon na Niger katika kupambana na wanamgambo wa Boko
Haram. Wakati huohuo siku ya Alkhamisi vyombo vya kijeshi vya Nigeria
vilitoa habari za kusafishwa baadhi ya miji ya majimbo matatu ya
kaskazini mashariki mwa Nigeria kutokana na magaidi hao wa kitakfiri.
Badhi ya miji hiyo ni mji wenye wakazi wengi wa Kikristo wa Madagali
ambao ulitekwa na kudhibitiwa na Boko Haram mwezi Agosti mwaka uliopita.
Akizungumza hivi karibuni na waandishi, Rais Goodluck Jonathan wa
Nigeria ametabiri kuwa majimbo mawili ya Adamawa na Yobe yatakombolewa
katika kipindi cha majuma mawili yajayo na jumbo la Borno katika juma la
tatu. Majimbo hayo yalikuwa chini ya sheria kali ya kutotoka nje usiku
sheria iliyotangazwa tokea mwezi Mei mwaka 2013. Rais Jonathan alitaka
kurefusha kwa mara ya tatu muda wa hali hiyo ya hatari katika majimbo
hayo matatu mwezi Novemba uliopita lakini hatua hiyo ikapingwa vikali na
wabunge. Hivi sasa operesheni za pamoja zinaendeshwa na askari wa
Nigeria, Cameroon, Chad na Niger kwa lengo la kurudisha amani na usalama
katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria kabla ya kufanyika
uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika nchini humo tarehe 28 mwezi huu.
Kutangaza kundi la Boko Haram kuwa linafungamana na kundi jingine la
kigaidi la Daesh kumeongeza wasiwasi nchini Nigeria wa kundi hilo
kufanya mashambulio makubwa ya kigaidi katika maeneo tofauti ya nchi
hiyo na katika maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na nchi jirani katika siku
zijazo. Kwa msingi huo viongozi wa nchi jirani ambazo zimeunda muungano
wa kieneo dhidi ya Boko Haram wana hamu kubwa ya kuona kuwa rasimu
iliyowasilishwa na nchi tatu za Nigeria, Chad na Angola inapitishwa
haraka iwezekanavyo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment